
Takriban wanajeshi 51 wameuwawa katika shambulizi la kushtukiza linaloshukiwa kufanywa na wanajihadi kaskazini mwa Burkina Faso.
Jeshi la nchi hiyo imesema washambuliaji 160 walifariki dunia katika mashambulizi ya kujibu mapigano. Shambulizi la kushtukiza lilifanyika ijumaa katika jimbo la Oudalan karibu na mpaka wenye vurugu wa Mali na Burkina Faso. Mpaka kufikia mwishoni mwa jana jumatatu, miili mipya 43 ilipatikana, na kufanya idadi ya awali ya vifo vya wanajeshi kufikia 51.
Idadi hiyo ya vifo iliongezwa kwenye takwimu ya awali ya vifo vya wanajeshi wanane iliyotolewa na jeshi jana jumatatu asubuhi. Jeshi liliongeza kusema kwamba operesheni zinaendelea kwa kuongezeka mashambulizi ya anga ambayo viliwezesha kudhibiti magaidi 100 na kuharibu zana zao. Burkina Faso inapambana na wanamgambo wenye msimamo mkali walioenea kutoka nchi jirani ya mali toka mwaka 2015. Ghasia hizo zimesababisha vifo zaidi ya 10,000, kulingana na makadirio ya mashirika yasiyo ya kiserikali na kusababisha watu milioni mbili kuyahama makazi yao.
Hasira ndani ya jeshi za kushindwa kukomesha umwagaji damu zimesababisha mapinduzi mawili mwaka jana.