
Manispaa moja nchini Afrika Kusini imesema itawaadhibu baadhi ya wafanyakazi wake kwa utovu wa nidhamu baada ya picha zao kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha wakiwa wamekaa na kulala juu ya makaburi.
Wafanyakazi hao wanatoka katika idara ya bustani za manispaa – ambayo ina jukumu la kusafisha bustani na vituo vya umma. kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Haijulikani ni lini picha hizo zilipigwa.
Katika taarifa hiyo manispaa ya Msunduzi, katika jimbo la Kwa-Zulu Natal, ilisema inafahamu kile ilichokiita “picha za kutatanisha”.
“Manispaa haitakubali tabia hiyo na inaweza kuthibitisha kuwa taratibu zipo kwa watumishi waliohusika kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu na kuiweka manispaa katika sifa mbaya,” ilisema.
Manispaa ilisisitiza kwamba watu hushikilia makaburi na mawe ya kaburi kwa heshima kubwa sana, kama mahali pa kiroho ambapo wanaheshimu kumbukumbu za wapendwa wao, na picha za watu walioketi na kulala juu yake ni ishara ya kutoheshimu.
Hii si mara ya kwanza kwa wafanyakazi kutoka mji mkuu wa KZN kukamatwa katika mazingira tatanishi.
Picha za awali zimewaonyesha wafanyakazi wa idara hiyohiyo wakiwa wamelala mchana, huku wengine wakipika chakula wakati wa kazi, jambo lililoibua wasiwasi kuhusu tija yao.