
Idadi ya waliofariki dunia kutokana na kimbunga Freddy nchini Malawi imeongezeka na kufikia vifo 326 na kufanya jumla ya vifo kufikia zaidi ya 400 tangu Februari mwaka huu.
Rais wa taifa hilo Lazarus Chakwera amesema vifo vimeongezeka kutoka 225 hadi 326, idadi ya wasio na makazi ikifikia 183,159.
Chakwera ametoa wito wa msaada wa kimataifa huku waokoaji wakiendelea kutafuta manusura kutokana na mafuriko na maporomoko ya matope yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha juma hili.
Kimbunga hicho kilirejea katika eneo la bahari ya hindi, kikakusanya nguvu kutokana na joto la maji na kuanza tena kufanya athari katika maeneo ya watu.