
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amekataa ombi la uongozi wa jimbo la Gauteng la kutaka rapa AKA wa nchi hiyo afanyiwe mazishi ya kitaifa.
Rapa AKA ambaye jina lake halisi ni Kiernan Forbes alifariki dunia jumamosi iliyopita baada ya kufyatuliwa risasi kutoka kwenye gari akiwa amesimama nje ya mgahawa muda mfupi kabla ya kutumbuiza jijini Durban.
Vyombo vya habari nchini Afrika Kusini vimeandika kuwa kiongozi wa Gauteng, Panyaza Lesufi alimuandikia Rais Ramaphosa kumtaka aridhie ombi ili rapa huyo maarufu nchini Afrika Kusini afanyiwe mazishi ya kitaifa.
Lesufi amesema hawakuitaka serikali kugharamia mazishi ya kitaifa ya AKA, lakini walichotaka jeneza litakalobeba mwili wake lizungushiwe bendera ya taifa na bendera zote za Afrika Kusini zipeperushwe nusu mlingoti ili kuenzi mchango mkubwa uliotolewa kwa taifa hilo na rapa huyo aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 35.