
Msanii wa Marekani, Robert Sylvester Kelly maarufu kama R Kelly amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa uhalifu wa kingono dhidi ya watoto.
Jaji wa shirikisho ameamua kuwa R Kelly atatumikia kifungo hicho kwa wakati mmoja na miaka 30 anayotumikia sasa. Ilikuwa ni jana alhamisi februari 23, ambapo hukumu hiyo ilitangazwa baada ya mahakama ya Chicago kumpata mwimbaji huyo na hatia ya mashtaka sita kati ya 13 yaliyoletwa dhidi yake mnamo septemba 2022.
Haya yalijumuisha mashtaka matatu ya kuwalazimisha watoto kufanya ngono haramu na pia makosa matatu ya kurekodi mkanda wa ngono ambayo yalimuonyesha akimdhulumu mtoto mdogo kingono.
R Kelly kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya ulaghai na ulanguzi wa ngono. Waendesha mashitaka walidai kwamba kifungo cha R Kelly kinapaswa kuongezwa juu ya kifungo anachotumikia sasa, wengine wakishauri afungwe jela maisha yake yote.