
Msichana mwenye umri wa miaka 17 ambaye aliripotiwa kufariki baada ya kushambuliwa na kupigwa na kundi la wenyeji kwa madai ya kuiba ndizi katika Mji wa Apac, Uganda, alipatikana akiwa hai katika chumba cha kuhifadhia maiti, saa chache kabla ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi.
“Taarifa ilipokelewa kwamba alifariki baada ya kupigwa na kundi la watu waliokuwa wakimtuhumu kwa wizi. Maafisa wetu walitembelea eneo la tukio, wakarekodi taarifa na kufikisha mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali kuu ya Apac,” msemaji wa polisi wa eneo la Kyoga Kaskazini, Bw Patrick Jimmy Okema, alisema.
Hata hivyo, wakati madaktari wakijiandaa kumfanyia uchunguzi wa kifo, waligundua bado alikuwa hai. Ipasavyo, alipelekwa wodini kwa mashine ya kusaidia maisha na bado anafuatiliwa.
Wakati huo huo, Bw Okema alisema tayari wana mtu mmoja kizuizini kwa madai ya kuhusika katika shambulio hilo la umati.
“Tunatoa wito kwa umma kuacha kuchukua sheria mkononi… Afadhali wawakamate na kuwakabidhi washukiwa wahalifu kwa polisi kwa hatua zinazofaa,” alisema.
Aliwaonya wanaokimbia kujisalimisha kwa polisi kabla ya kuwindwa.
“Wanaokimbia wajue tumewaweka wazi, hivyo wajitoe tu polisi na kujibu tuhuma za kujaribu kuua, kabla hatujawasaka,” aliongeza