
Mawaziri wa fedha wa kundi la nchi zilizotawi kiuchumi, G7 wamelitaka shirika la fedha la kimataifa (IMF) kutoa kifurushi kipya cha msaada kwa Ukraine kufikia mwisho wa mwezi machi, kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa alhamisi baada ya mkutano huko Bangalore, India.
Wakati huo huo Ujerumani imeandaa msururu wa hatua zinazolenga kuziba mianya ya vikwazo vya umoja wa Ulaya dhidi ya Moscow, hususani kuzuia bidhaa zilizowekewa vikwazo kuendelea kuingia Urusi kupitia ya nchi tatu.
Berlin itashinikiza hatua hizo ziwe sehemu muhimu ya duru ya 11 ya vikwazo vya umoja wa Ulaya dhidi ya Moscow, wizara ya uchumi imesema kifurushi cha 10 cha vikwazo vya umoja wa Ulaya kitatangazwa leo ijumaa, siku ya kumbukumbu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.