
Marekani imetangaza zawadi ya dola milioni tano kwa mtu atakayetoa taarifa itakayosaidia kukamatwa kwa Seka Musa Baluku, kiongozi wa wanamgambo wa kundi la Islamic State adf katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
Kiongozi anayesakwa wa ADF ni raia wa Uganda ambaye huenda ana umri wa miaka 40 kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Chini ya uongozi wa Seka Musa Baluku, kikundi hicho kinalenga, kuua, kulemaza, kubaka, na kufanya ukatili mwingine wa kingono na kushiriki katika utekaji nyara wa raia, wakiwemo watoto.
Kundi hilo pia huajiri na kuwatumia watoto wakati wa mashambulizi na kazi ya kulazimishwa katika eneo la beni mashariki mwa DR Congo.
Kundi hilo linatuhumiwa kuwaua maelfu ya raia wa kongo na kutekeleza mashambulizi ya mabomu nchini Uganda.
Mwaka 2020 pekee, kundi hilo linasemekana kuwaua zaidi ya raia 849, kulingana na baraza la usalama la umoja wa mataifa.