
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ameitaka klabu hiyo kukubali kumuongeza mkataba mpya mshambulizi raia wa Ufaransa, Karim Benzema, pamoja na kusisitiza kuwa mshambuliaji huyo mkongwe wa ufaransa hatakwenda popote katika majira ya joto.
Benzema anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji mabao wa muda wote wa Real nyuma ya Cristiano Ronaldo pekee na mbele ya Raul na Alfredo Di Stefano.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 ameifungia Real Madrid mabao 202 katika kipindi cha miaka minne na nusu pekee iliyopita na pia aliteuliwa kuwa nahodha wa klabu kufuatia kuondoka kwa Marcelo majira ya joto.
Msimu huu umekuwa mgumu kidogo kwa sababu ya majeraha, lakini Benzema bado amekuwa akifunga anapopata nafasi ya kucheza. Mkataba wa Karim Benzema unamalizika msimu ujao wa joto na Ancelotti ametilia mkazo kuwa nyota huyo wake kubaki.