
Wakati wafugaji nchini wakilalamika kukosa tija katika sekta hiyo, serikali imetumia Tsh 3.5 bilioni kununua mbegu ya madume ya Ng’ombe na mitamba aina ya Boran Heifer kwa ajili ya kuwagawa kwa wafugaji katika halmashauri nane nchini kama mbegu ili kuongeza uzalishaji wa Ng’ombe wa nyama na maziwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Ng’ombe dume 36 aina ya Boran Heifer kwa vikundi vya wafugaji kutoka halmashauri ya Buchosa, naibu Waziri wa mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega amesema Ng’ombe hao ni sehemu ya Ng’ombe dume 366 watakaogawiwa kwa wafugaji katika halmashauri nane za mfano nchini.
Ulega amesema madume hayo yenye sifa ya kuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na Ng’ombe wa kienyeji wana uwezo kwa kukua ndani ya muda mfupi na kuihakikishia nchi uwepo wa mazao yatokanayo na Ng’ombe ikiwemo malighafi za viwanda nchini.